Swahili NT 1Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.
2Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
3Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
4Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
5Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda. 6Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, 7ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. 8Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. 9Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. 10Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. 11Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. 12Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu. 13Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao. 14Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. 15Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa." 16Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo. 17Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo. 18Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu. 19Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?" 20Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, "Mimi siye Kristo." 21Hapo wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?" Yohane akajibu, "La, mimi siye." Wakamwuliza, "Je, wewe ni yule nabii?" Yohane akawajibu, "La!" 22Nao wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma." 23Yohane akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana." 24Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. 25Basi, wakamwuliza Yohane, "Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?" 26Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado. 27Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake." 28Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza. 29Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu! 30Huyu ndiye niliyesema juu yake: Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa! 31Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua." 32Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake. 33Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu. 34Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu." 35Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili. 36Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu." 37Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu. 38Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?" 39Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni. 40Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu. 41Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha" (maana yake Kristo). 42Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani, "Mwamba.") 43Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, "Nifuate." 44Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro. 45Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, "Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti." 46Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?" Filipo akamwambia, "Njoo uone." 47Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, "Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake." 48Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje kunijua?" Yesu akamwambia, "Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona." 49Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!" 50Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya." 51Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu." Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE. Bible Hub |