Yohana 15
Swahili NT
1Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 2Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi. 3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni. 4Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. 5Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote. 6Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue. 7Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa. 8Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu. 9Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu. 10Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike.

12Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi. 13Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi chochote mumwombacho kwa jina langu. 17Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: pendaneni.

18Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla haujawachukia ninyi. 19Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi kama watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni. 20Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia. 21Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma. 22Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi. 23Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia. 24Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakinichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia. 25Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika Sheria yao: Wamenichukia bure!

26Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

John 14
Top of Page
Top of Page